Enter your keyword

Culture for Life.

Showing posts with label lugha. Show all posts
Showing posts with label lugha. Show all posts

Saturday, September 16, 2017

NATARAJIA KUINGIZA SOKONI KITABU CHANGU HIVI KARIBUNI KINACHOKWENDA KWA JINA "MAPENZI KABURINI"

By On September 16, 2017
 

 

Ningependa ujue kipaji hiki kimeanzia wapi?

Huwa napenda  kujibembeleza au kujifariji nikiwa natembea kwa kutengeneza hadithi katika fikra zangu ili kuweza kufika ninakoelekea bila kuchoka au ninapotaka kulala,Vilevile kipindi nikiwa shuleni nilikuwa napenda sana kutengeneza hadithi na kuweza kuziigiza wakati wa mahafali na wanafunzi wenzangu ingawa wakati mwingine wenzangu walinicheka na kuniona ninakihelehele lakini sikukata tamaa.Hata nilipoendelea na elimu yangu ya chuo kikuu kipaji,hakikuishia hapo niliendelea kutunga hadithi na kuzihifadhi.

Siku moja baada ya kushiriki shindano la uandishi wa Riwaya fupi kwa wanafunzi wa shule ya msingi,sekondari na vyuo vikuu Tanzania kwa ajili ya Tuzo ya mama Salma Kikwete iliyoandaliwa na  TASAKI(Tamasha la Sauti ya Kiswahili) niliibuka mshindi wa pili wa riwaya fupi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu Tanzania mwaka 2010.

Hivyo hiki kitabu ni muendelezo wa Riwaya niliyopatia Tuzo.Soma kitabu hiki uweze kujionea ubunifu wa hali ya juu wa fani pamoja na mshikamano wa maudhui uliyopo ndani ya kitabu hiki.

Mapenzi Kaburini ni kitabu chenye mtazamo yakinifu,ni kitabu ambacho maudhui yake yamezitazama nchi za Afrika  na changamoto zilizopo katika nchi kwa upande wa viongozi pamoja na wananchi.Kimebeba maudhui yanayowalenga wananchi wote bila kujali utabaka.Kwa upande wa fani kimetumia majina ya halisi na kubuni hasa kwa upande wa maeneo ya miji mfano kuna miji kama Kinyonga,kupe,chatu ambayo ni majina yaliyopo katika nchi ya Simba.Nchi hii ya Simba ni nchi inayosimamia nchi zilizopo Afrika Mashariki.

Mbali na hilo pia visa na matukio vimepewa majina ya hifadhi za Taifa zilizopo katika nchi ya Tanzania.Mfano hifadhi ya Ruaha,Sanane,Manyara na kitulo kama ukisoma kitabu hiki utagundua kuwa sifa ya hifadhi inaendana na visa na matukio yaliyopo katika sehemu hiyo iliyoandikwa kwa jina la hifadhi.Mfano hifadhi ya Kitulo inasifika kwa kuwa  na maua,kama tujuavyo maua huashiria sifa nyingi moja wapo hapo ni upendo,watu wengi hutumia maua katika kuwapa wapenzi wao,mfano kuomba msamaha,kumfariji mtu,hata kuonesha upendo kwa mtu unayempenda.

Utakaposoma kitabu  hiki  utaburudika na kufundishwa baadhi ya mambo kama Kukuza imani yako kwa Mungu,uaminifu katika ndoa,uzalendo katika nchi yako na Madhara ya kujihusisha katika mahusiano  na mtu usiye mjua.

Nitakupatia kionjo kidogo katika sura ya kwanza ili kuweza kuona mwanzo tu wa hadithi hii ambayo hutapenda kuacha kuifuatilia:

 

Sura ya kwanza 

 Hifadhi ya Sanane  

Ilikuwa siku ya Jumatatu katika ghorofa la tajiri mmoja, mmiliki wa hoteli maarufu katika nchi ya Simba. Tajiri huyo alifahamika  sana kwa kuwa alikuwa akijitolea sana kwa wananchi wasiojiweza, katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.Watu husemamfadhili  punda kuliko mwanadamu vilevile  tenda wema kisha nenda zako baraka utazipata kwa Mungu,usisubiri hisani  za wanadamu.

 Pamoja na misaada aliyoitoa kwa watu mbalimbali lakini wananchi wa Simba hawakujali misaada yake, walimteta kila kona kuwa anatumia nguvu za giza na amekwisha toa kafara ndugu, jamaa na hata watoto wake ili kujipatia utajiri mkubwa alionao. Siku hiyo ya Jumatatu katika pagala  la tajiri huyo aliyefamika kwa jina la Pesa nyingi.

 katika moja ya chumba cha ghorofa hilo kulikuwa na mwanamke mrembo na mzuri sana wa sura, mrefu mithili ya twiga, mwenye umbo zuri la kiafrika, chini alikuwa amevaa suruali ya chupa huku akiwa amevaa blauzi tatu juu zenye rangi tofauti na nywele timutimu zikiwa zime nakishiwa na vitu vya jaani kama vichana,visude, rasta chakavu na kufungwa kitambaa cha kitenge aina ya makenzi ,uso wake ulikuwa kama paka mwenye madoa kutokana  na kujipamba kwa majivu na masizi ya mkaa wa jaani. Pembeni ya ua hilo alikuwepo mnyama mwenye maringo

mbugani kuliko wote, sio mwingine bali ni kijana mtanashati aliyekwenda hewaani, rangi ya ngozi yake   nyeusi ya kung’aa. Tabasamu la mwanaume huyo lililokuwa likimfariji mtoto mzuri, lili mvutia sana Savannah. Ghafla ilisikika sauti ya mwanamke huyo ikiita kwa sauti ya chini iliyojaaa simanzi na mateso ya muda mrefu,ilisema “John naumia mume wangu, hali yangu kila kukicha afadhali ya jana”. 

John alijibu  “usijali Savannah nipo hapa mke wangu kwa ajili yako utapona tu tutakwenda hospitali,subiri  nikuandalie chakula ule, kisha nikupeleke hospitali  malikia wangu”. Basi baada ya John kumfariji Savannah aliamka na kuelekea jikoni pembeni ya sehemu aliyokuwa amelala mpenzi wake. Watu hawa walipendana sana ni vile tu hali yao haikuwa nzuri kifedha waliishi kwa kuhangaika, kuomba msaada na wakati mwingine walifukuzwa na walimwengu pale walipokuwa wakiomba msaada, watu waliwapita kama mbwa waliokosa matunzo. 

Wapenzi hao Walizoea maisha ya kuokota vyakula jalalani na kukimbilia magari ya taka sambamba na kusubiria mabaki ya chakula katika migahawa mbalimbali. Wakati huo John alikuwa akitimiza ahadi aliyo mhahidi malikia wake alimuandalia chakula walicho kiokota katika soko kuu la mji huo wa Chatu. John alimuinua Savannah pale alipokuwa amelala kwenye kanga chakavu akiwa amejifunika magunia yalionekana ni ya mpunga. John alimlisha Savannah chakula kile ambacho hawakujua kilipikwa lini na kutupwa na nani na lini. Savannah alisikika akisema “asante mume wangu hata

mwanangu anafurahi sasa naona napata nafuu, nahisi ni njaa ilikuwa inaniuma”. Mwanangu nisamehe mama kakushindisha njaa, nakupenda sana najua wewe utakuwa mrembo zaidi yangu mwanangu hata baba yako anakupenda”. John alikuwa anapenda sana utani alicheka na kusema “atakuwa mrembo kama wewe kweli mke wangu lakini rangi ya ngozi yake itakuwa kama yangu, yako iko kama ya nguruwe hahahaaaa!” Savannah alikuwa mweupe kama Nguruwe, ingawa alivyokuwa anaonekana ni kama mtu mwenye  ngozi  ya rangi ya maji ya kunde kutokana na ugumu wa maisha. 

Wawili hao walifurahi pamoja na kusahau shida walizokuwa nazo.Walipomaliza kula wapenzi hao waliamua kutoka  nje baada ya kukaa ndani ya paghala hilo kwa muda wa wiki moja, Dikidiki hao walikuwa na kaida ya kufanya hivyo wanapotafuta riziki na kujilimbikizia ndani ya paghala lao kisha wana kaa kwa muda huo bila kutoka. Usilolijua ni  kama usiku wa kiza, basi Savannah na John walipotoka  wakiwa n’je ya mgahawa mmoja uliokuwa unapendwa sana na wananchi wa mji huo wa Chatu zilisikika sauti za wanawake wakisema: 

“haya  jamani sasa ni ule wakati wa Pesa nyingi kuingiza hela sasa wenzi wametoka fungate”. Waliamini kuwa Pesa nyingi alikuwa anawatumia Dikidiki hao  kama misukule inayotoka na kurudi ndani na wanapotoka basi  mzee Pesa nyingi huingiza hela nyingi sana. Kwakuwa wenzi hao walikuwa hawaelewi kinachoongelewa waliendelea kuomba msaada kwa wateja waliokuwepo hapo mgahawani. Wanapokosa waliamua kucheza baadhi ya nyimbo zilizokuwa

zikipigwa katika mgahawa huo, wakicheza hupewa chakula na fedha ambazo hutoka katika mifuko ya wateja. John alikuwa anapenda sana kucheza,wakiwa wamekaa chini walisikia wimbo wa mwanamuziki maarufu Tanzania Diamond unaosema Je, Utanipendaga? John alimuinua Savannah aliyeonekana kachoka na mimba yake. Savannah aliamka na kucheza na mpenzi wake ,walicheza kwa  miondoko ya kihindi, machozi yalisafisha uso wa Savannah huku yakiosha kifua cha John kilichokuwa kimejaa kama mlima na mikono iliyokuwa na miinuko ya kupanda na kushuka ilizunguka juu ya  kifua cha Savannah na kumfanya ahisi kazungukwa na jeshi kubwa la malaika wa ulinzi.

 Baada ya kumaliza kucheza savannah alikuwa amechoka sana, kitendo cha kucheza kilimsababishia kuchokoza maumivu na kupelekea kupata uchungu katika kizazi chake. Baada ya kuona hivyo John aliinama na kuchukua zawadi walizozipata kutoka kwa hadhira iliyokuwa ikiwatazama huku baadhi ya hadhira wakibubujikwa na machozi walimpelekea hela na chakula John katika kapu lake la kukusanyia riziki. Watu waliokuwa wakiwatazama Savannah na John hawakujali maumivu ya mwanamke yule na kuona kawaida. 

Wapo waliosikika wakisema hawa vichaa wana akili, wengine walisema hawa si vichaa, vichaa gani wana akili ya kutafuta hela hivi, wamekusanya umati mkubwa hivi na kuwafanya watu kutoa kile walichonacho. Mama mmoja mwenye busara anayeuza katika mgahawa huo aliyefahamika kwa jina la mama ndaga akasema“Jamani mimi nawafahamu hawa vichaa kwanza hawakuwa wakitembea hivi pamoja kama Dikidiki, huyo kaka unayemuona alikuwa..........pata mwendelezo kwa kujipatia kitabu hiki.

Nicheki kwa mawasiliano haya:+255756377940

                                    intagram:sinyatiblog

                                     facebook:Tupokigwe Abnery

 

Monday, March 27, 2017

Dhamira alizozimulika Mwanamziki Ney wa Mitego katika wimbo wa "WAPO"

By On March 27, 2017

 

 Mwanamuziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki,

Dhamira zilizopo  katika wimbo wa msanii Ney wa mitego wapo
Napenda kutoa pongezi zangu kwa Raisi wetu Dkt..John Pombe Magufuli kwa kuruhusu huu wimbo kupigwa katika vyombo vya habari vilevile kumtaka msanii huyu kuongeza maudhui mengine katika wimbo huu ili kuielimisha jamii,Pili pongezi zangu ziende kwa msanii huyu wa mziki wa kizazi kipya  Ney wa mitego kwanza kabisa kwa kutumia lugha ya Kiswahili katika wimbo wake kwani unasaidia sana kuikuza lugha ya Kiswahili pia kwa kutumia lugha raihisi ambayo inaeleweka kwa jamii.

Msanii ni kioo cha jamii na ni daraja la jamii,Katika wimbo huu binafsi amenigusa sana kwani wasanii wengi wamejikita katika maudhui ya mapenzi na kusahau matatizo yanayoikabili jamii vilevile ni mfano wa kuigwa kwa wasanii wengine pamoja na kuwa fundisho kwa wasanii wengi kuwa wabunifu zaidi katika uwasilishaji wa maudhui ya wazingatie zaidi kipengele cha fani ili kiende sanjari na maudhui.

Kwa ujumla msanii Ney wa Mitego ameweka wazi matatizo yaliyopo katika jamii katka nchi nyingi.Nikianza na maudhui nita zitaja dhamira ndogondogo zilizojitokeza katika wimbo huu

       i.            Kufanya kazi kwa bidii,” uchopanda leo ndiyo utakachovuna kesho”.

     ii.            Matumizi ya madawa ya kulevya na ukabaji,mfano wasanii mateja,wanafunzi vyuo vikuu na viongozi wanaotumia madawa ya kulevya.

  iii.            Uhuru wa kuzungumza mf vyombo vya habari

  iv.            Suala la uwajibikaji kwa viongozii

     v.            Suala elimu mf kutumia vyeti bandia

  vi.            Mmomonyoko wa maadili mf  {mademu } wanawake kusagana,Biashara ya ngono,mambo hayo yapo kinyume na utamaduni wetu na si kwa wanawake tu bali hata wanaume wanaojihusisha na ushoga ni vema kuacha na kuzingatia maadili.

vii.            Mila na desturi potofu mf wasanii kulogana,wanaume kulelewa

Nay wa Mitego baada ya kuachiliwa huru



Friday, March 10, 2017

NADHARIA TETE NA HALISI ZA ASILI YA LUGHA KISWAHILI.

By On March 10, 2017


Ndani ya hifadhi ya Momela-Arusha- Tanzania

 Kiswahili Asili Yake ni Kongo
Baadhi ya wataalamu hudai kuwa asili ya lugha ya Kiswahili ni huko Kongo ambayo baadaye iliitwa Zaire na sasa inaitwa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo. Dai hili linaimarishwa na wazo lingine linalodai kwamba katika vipindi kongwe vilivyopata kuwako, sehemu za Pwani ya Afrika mashariki hazikuwa zimekaliwa na watu. Kutokana na hali ya vita, uchungaji na biashara, inadaiwa kuwa Wabantu walitoka sehemu za Kongo walisambaa na kuja pwani ya Afrika mashariki kupitia Kigoma. Baadhi ya wabantu hawa walipitia sehemu za Uganda. Wakati wa kusambaa kwao, walieneza pia lugha zao ikiwemo hii ya Kiswahili.

Udhaifu wa nadharia hii ni kwamba, madai ya kuwa asili ya Kiswahili ni Kongo hayana msingi kwani mpaka sasa wataalamu wanaodai hivi hawajaweza kueleza na kuthibitisha kisayansi ama Kihistoria juu ya lini hasa watu walianza kuishi pwani ya Afrika mashariki.

  Kiswahili ni Ki-Pijini au ni Ki-Krioli

(i)     Kiswahili ni Ki-Pijini
Baadhi ya wataalamu hudai kuwa Kiswahili ni Ki-Pijini. Wataalamu hawa hudai kwamba Ki-Pijini ni lugha ambayo huzaliwa kutokana na kukutanika  kwa makundi mawili (A) na (B) yanayotumia lugha mbili tofauti. Ili makundi haya yaweze kuwasiliana kunaundwa lugha ambayo kitabia ni tofauti  na zile zinazozungumzwa na makundi yanayohusika. Lugha hii inaweza kuwa na msamiati mwingi kutoka lugha kati ya zile mbili, au inaweza kuwa na msamiati wenye uzito sawa. Lugha hiyo ndiyo inayoitwa Ki-Pijini. Mazingira yanayosababisha kuwepo Ki-Pijini ni kama vile biashara, utumwa, ukoloni, nk.
Kwa mantiki ya nadharia hii, wataalamu hawa hukiona Kiswahili kuwa kilianza kama Ki-Pijini kwani ni tokeo la mwingiliano baina ya wenyeji wa pwani ya Afrika Mashariki na wageni wa kutoka Mashariki ya Kati, hususan Waarabu. Aidha, husisitiza kuwa lugha ya Kiswahili haikuwepo kabla ya hapo.
(ii)    Kiswahili ni Ki-Krioli
Wataalamu hawa wanadai kwamba watu wanaozungumza Ki- Pijini wanaweza kuishi pamoja kwa muda wa karne nyingi na kwa hiyo wakaweza kuzoeana na hata kufikia hatua ya kuoana. Wakioana watoto wao huikuta lugha ya ki-Pijini ama lugha yao ya kwanza. Inapofikia hatua ya aina hii kwa watoto wanaozungumza lugha hiyo, wao husemekana sasa  wanazungumza lugha ya Ki-Krioli, lugha ambayo ni hatua ya juu ya Ki-Pijini, yaani Ki-Pijini kilichokomaa.

Nadharia hii hutumia kigezo cha msamiati wa Kiswahili kuonesha uhusiano uliopo kati ya Kiswahili na Kiarabu. Wanadai kuwa, msamiati mwingi wa Kiswahili unatokana na Kiarabu. Hivyo huhitimisha kuwa hapana shaka Kiarabu kimehusika katika kuizalisha na kuikomaza lugha ya Kiswahili.

Udhaifu wa nadharia hii ni kwamba hutumia kigezo cha msamiati tu bila kuzingatia vipengele vingine vya lugha kama vile matamshi, maumbo ya maneno au muundo wa sentensi za Kiswahili. Aidha, wataalamu hawa hawakuhoji suala la kufanana kwa Kiswahili na lugha jirani katika hayo yaliyotajwa hapo juu na katika eneo la Kijografia ambamo Kiswahili na lugha hizo nyingine hujikuta zikizungumzwa. Vigezo hivi ni ushahidi tosha unaoonesha kuwa Kiswahili SI Ki-Pijini wala SI Ki-Krioli, bali ni lugha kama zilivyo hizo lugha jirani.
  Kiswahili ni Lugha ya Jamii ya Vizalia
Kundi la kwanza la wataalamu wa nadharia hii, Bishop Edward Steera, Bwana Taylor, Dkt. R. Reusch, (Katika Maganga, 1997)  hudai kwamba:
·        Waarabu na Waajemi waliohamia pwani ya Afrika ya Mashariki waliwaoa wanawake wa  ki-Afrika.
·        Watoto wao walijifunza maneno ya Kiarabu na ki-Ajemi kutoka kwa baba zao.
·         Aidha, watoto hao wakajifunza maneno ya ki-Bantu kutoka kwa mama zao.
·        Katika jitihada zao, watoto hao walijirekebisha kutokana na  tamaduni za wazazi wao ambazo ni tafauti: utamaduni wa Kiarabu na utamaduni wa ki-Bantu.
·        Vizalia hawa wakaanza kutumia lugha mpya ya mseto wa Kiarabu, Kiajemi na lahaja mbalimbali za ki-Bantu.
·        Kwa kiasi kikubwa, lugha mpya ya mseto ilikuwa ni upotoshaji wa lugha ya Kiarabu na Kiajemi.
·        Mwarabu au Mu-Ajemi alikuwa muumini wa dini ya Uislamu.
·        Umo humo, vizalia hawa wakayaingiza maneno ya Kiarabu, Kishirazi na Kihindi katika hii lugha mpya.
·        Pamoja na kuyaingiza maneno ya kigeni, lugha-mpya yao hii (Kiswahili), ilikithiri vionjo vingi vya lugha mbali mbali za ki-Bantu.
·        Ndipo baadaye, lugha mpya yao hii ikajulikana au kuitwa Kiswahili.
·        Kwa maoni ya wataalamu hawa, sehemu mbili kati ya tano (2/5) ya maneno yanayotumika katika lugha hii mpya ni ya ki-Bantu.
·        Sarufi ya lugha mpya hii ni mseto wa ki-Bantu (chenye utata na kisicho na mpangilio maalumu) pamoja na Kiarabu (chenye mantiki na kilichokomaa).
          
Kundi la pili la wataalamu wa nadharia hii, B. Krumm na F. Johnson lina mawazo yanayodai kwamba:
·        Kiswahili kilitokana na visiwa vya Lamu, Kilamu/Kiamu.

·        Wageni kutoka Ghuba ya Ushirazi/Uajemi na Arabia ya Kusini walikuja katika Pwani ya Afrika ya Mashariki na lugha tofauti.

·         Lakini kutokana na kuoana kwao na wenyeji, wageni hawa wakaichukua lugha ya hapo walipofikia, wakaikuza kwa maneno kadhaa na sentensi kadhaa kutoka lugha zao za asili, yaani Kiarabu, Kiajemi na Kihindi hususan katika masuala ya  biashara, ubaharia, vyombo vya kazi zao na nguo.
·        Aidha,  utumwa na tabia ya kuoa wake wengi ilisaidia kutoa kundi kubwa la masuria. Hali hii ikaondosha hisia za ugeni katika lugha zao; na maneno yote yakabatizwa kuwa ya ki-Bantu, na hata kupoteza kabisa sura ya ugeni.
   Kiswahili ni Kiarabu
Kuna hoja kuu tatu ambazo baadhi ya wananadharia hii huzitumia kutetea nadharia hii kuwa Kiswahili asili yake ni Kiarabu.
(i)          Inadaiwa kuwa maneno yenye asili ya Kiarabu yaliyomo katika Kiswahili ni ishara tosha kwamba lugha hii ilianza kama Pijini ya Kiarabu.
(ii)       Inahusu neno lenyewe Kiswahili ambalo asili yake ni Kiarabu. Neno Kiswahili linatokana na neno “sahili” (umoja) na “swahil” (wingi) lina maana ya pwani.
(iii)     Inadaiwa kwamba kwa kuwa Kiswahili kilianza pwani, kwa kuwa idadi kubwa sana ya wenyeji wa pwani ni waislamu, na kwa kuwa uisilamu uliletwa na Waarabu, basi Kiswahili nacho kililetwa na Waarabu.
   Kiswahili si Kiarabu
Madai kwamba Kiswahili si Kiarabu yanathibitishwa na hoja kinzani zifuatazo:
Tukianza na dai la kwanza ‘kwamba maneno yenye asili ya Kiarabu yaliyomo katika Kiswahili ni ishara tosha kwamba lugha hii ilianza kama pijini ya Kiarabu’ tunaona wazi kwamba madai haya hayana mashiko. Lugha ya Kiswahili imetokea kuwa na maneno ya mkopo yenye asili ya Kiarabu (na kwa hakika yapo yenye asili ya Kiajemi, Kireno, Kihindi, Kijerumani, Kiingereza
 kutokana na ukweli kwamba kulikuwa na mawasiliano ya karne na karne baina ya wenyeji wa pwani na wafanyabiashara wa Kiarabu. Wasemaji wa lugha mbili tofauti wanapokutana hawaachi kuathiriana kilugha. Kwa hiyo lugha kuwa na maneno mengi ya mkopo kutoka lugha nyingine, haifanyi lugha hiyo isemekane kuwa imetokana na hiyo lugha nyingine.

Pili wataalamu hawa wanadai kwamba neno lenyewe Kiswahili lina maana ya Kiarabu.
Kwani linatokana na neno “sahili” (umoja) na “swahil” (wingi) lina maana ya pwani. Hapa ingetupasa tuelewe kwamba kila mtu binafsi au jamii binafsi aghalabu hajiiti mwenyewe jina lake, yeye huitwa kwa hilo jina alilopewa na wengine: Jamii yake au wageni waliomtembelea kwake. Na hivi ndivyo ilivyojitokeza kwa upande wa jamii ya watu wa pwani ya Afrika mashariki, yaani Waswahili,  walipotembelewa na Waarabu na kuitwa As-Sahilyy au As-Sawahiliyy, na nchi yao kuitwa sahil (wingi wake Sawahil), yaani pwani (upwa), ufuo. Kwa mantiki hii, dai hili halina mashiko !

Kigezo cha dini nacho hakikubaliki lugha haiwi lugha kwa sababu ya imani. Hata hivyo lugha ya Kiarabu yenyewe ilikuwepo karne nyingi kabla ya kufunuliwa dini ya Uislamu. Hali kadhalika, lugha nyingine za Kimagharibi zilikuwepo karne nyingi kabla ya kufunuliwa imani ya ukristo. Kama ilivyo kwamba Kiingereza au Kijerumani si ukristo, basi ndivyo vivi hivyo ilivyo kwamba Kiswahili hakiwezi kuwa dini ya uislamu, aslan! Wala Kiarabu nacho si uislamu. Tunachoweza kufanya ni kuitumia lugha kuifasili dini, lakini hatuwezi kuitumia dini kuifasili lugha.
 Kiswahili ni Kibantu
Vipengele vinavyotumika katika kuihalalisha nadharia inayodai kwamba Kiswahili ni Kibantu ni ushahidi wa ki-Isimu, ushahidi wa ki-Historia na kuichunguza lugha ya Kiswahili katika mfumo mzima wa historia ya mgawanyiko wa kusambaa kwa lugha za ki-Bantu. Wataalamu wa nadharia hii wanahitimisha kwa kudai kwamba Kiswahili ni mojawapo kati  ya lugha katika jamii kubwa ya lugha za ki-Bantu.
Baadhi ya wataalamu muhimu wanaoiunga mkono nadharia hii ni Prof. Malcon Guthrie, Dkt. C. Meinholf na Dkt. C. Rohl na Prof. Clement Maganga.

Profesa Malcom Guthrie
 Ni mtaalamu (mwanaisimu) mashuhuri kutoka Chuo Kikuu cha London, Uingereza. Alitumia miaka 20 kuchunguza uhusiano uliopo baina ya lugha za Kibantu zilizoko katika eneo lote ambalo hukaliwa na wabantu. Sehemu hii ni ile ambayo inajulikana kama Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Alifanya uchunguzi wa mashina/mizizi (viini) ya maneno 22,000 kutoka lugha 200 za Kibantu. Katika uchunguzi wake alikuta mizizi (mashina) 2,300 imezagaa       katika lugha mbalimbali za Kibantu na Kiswahili kikiwemo. Mashina/mizizi 500yalilingana katika lugha zote 200. Mashina haya yalipatikana katika lugha zote za Kibantu. Mashina haya yalikuwa ya asili moja. Baadhi ya lugha hizo 200 zilizofanyiwa uchunguzi Kiswahili kilionesha kuitikia ulinganifu sawa na Kikongo kwa asilimia arubaini na nne (44%).

Katika kuchunguza ni asilimia ngapi za mashina hayo 500 yaliyomo katika kila lugha, mgawo uliojitokeza ulikuwa kama ifuatavyo:

Kiwemba kizungumzwacho Zambia         -           54%
Kiluba kizungumzwacho Katanga             -           51%
**Kikongo kizungumzwacho Zaire           -           44%**
**Kiswahili kizungumzwacho Afrika Mashariki            44%**
Kisukuma kizungumzwacho Tanzania                 41%
Kiyao kizungumzwacho Tanzania/Msumbiji -   35%
Sotho kizungumzwacho Botswana                        -           20%
*Kirundi kizungumzwacho Burundi         -           43%*
Kinyoro kizungumzwacho Uganda           -           37%
Kizulu kizungumzwacho Afrika Kusini   -           29%

Baada ya kupata matokeo haya, Profesa Malcom Guthrie anaiunga mkono nadharia hii ya kwamba Kiswahili ni ki-Bantu kwa kudai kwamba:
(i)     Kiswahili kilikuwepo kabla ya ujio wa wageni;
(ii)    Anaonyesha kwamba Kiswahili kina uhusiano mkubwa na lugha za Kibantu;
(iii)  Mwisho anasema Kiswahili kilianzia Pwani ya Afrika Mashariki.
          
Dkt. C. Meinholf na Dkt. C. Rohl: Wataalamu hawa wanaamini kwamba:
(i)  Wakati wa utawala wa Shirazi katika upwa wa mashariki ya Afrika kulikuwa na kabila la Waswahili;

(ii)             Kabila hili ni dhuria ya Wazaramo wa leo.

(iii)           Kwa kuwa hawa Wazaramo walikuwa wamezaliwa katika harakati za kibiashara, kwa hivyo wakafuata nyayo za wazazi wao.

(iv)           Lugha yao ilikuwa ya aina ya ki-Bantu.

(v)              Kwa kuwa Wabantu ni wengi zaidi kuliko jamii ya makabila mengine, lugha yao ya Kiswahili ikaanza kutumika na kuenea katika makabila mengine, hususan katika ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki.

(vi)           Baadaye, Waswahili hawa hawa wakafanya biashara na wageni waliokuja kuvinjari Afrika Mashariki, hususan Waarabu, Washirazi, Wamalaysia, Wahindi na Wareno ambao tayari walikuwa wamefurika katika pwani hii ya Afrika Mashariki miaka kadhaa kabla.
(vii)         Vifaa na majina ya vitu vya biashara vya wageni hao vikaselelea na kuingizwa katika mfumo wa lugha hiyo ya Waswahili ambayo ni ki-Bantu.

Madai ya nadharia hii yakichunguzwa, tunagundua kwamba inazingatia mitazamo miwili yaani, mtazamo wa ki-Isimu na mtazamo wa ki-Historia. Kwa mantiki hii, nadharia hii inaelekea kukubalika na wataalamu wengi kuwa ndiyo sahihi kuhusu asili au historia ya Kiswahili.

Profesa C. Maganga, na uthibitisho wake kwamba Kiswahili ni ki-Bantu. Kama tulivyoona, lugha ya Kiswahili ilifanyiwa utafiti na uchambuzi na wanataaluma kadhaa kwa madhumuni ya kuiainisha kama ilikuwa yenye misingi ya ki-Bantu au la. Prof. Maganga alifanya uchambuzi wa ki-Isimu na wa ki-Historia kuhusu lugha hii. Matokeo ya utafiti wake wa ki-Isimu kuhusu lugha ya Kiswhili (au lugha kwa ujumla) unadhihirisha mambo mengi, mojawapo ni asili ya lugha hiyo. Amethibitisha kwamba Kiswahili ni lugha ya Kibantu; na kwa hivyo, kuthibitisha kwa ushahidi thabiti hoja ya Dkt. C. Meinholf na Dkt. C. Rohl kama  tulivyoieleza hapo juu.

(i)        Ushahidi wa Kiisimu
(a)      Msamiati
Matokeo ya utafiti alioufanya kuhusu msamiati wa Kiswahili ulibaini kwamba 60% ya maneno yote yanayoweza kuandikwa na kutamkika katika lugha ya Kiswahili asili yake ni lugha za Kibantu, 30% ni lugha ya Kiarabu na 10% ni lugha nyingine za kigeni kama vile Kiingereza, Kireno, Kijerumani, Kihindi, Kiajemi, Kifaransa, nk. Kinyume chake ni kwamba msamiati wa Kiswahili na ule wa Kibantu hautofautiani.

Mfano:
            Kiswahili   Kindali  Kizigua   Kijita   Kikurya   Kindendeule          
            Mtu          Umundu    Mntu       Omun      Omontu      Mundu
            Maji         Amashi      Manzi     Amanji    Amanche    Maache
            Moto        Umulilo     Moto        Omulilo   Omoro        Mwoto

 (b)      Tungo (Sentesi) za Kiswahili
Miundo ya tungo (sentesi) za maneno ya Kiswahili zinafanana sana na miundo ya tungo za maneno ya ki-Bantu. Sentesi za Kiswahili na za lugha za ki-Bantu zina kiima  na kiarifu.

Mfano:
Lugha za Kibantu               Kiima                         kiarifu
Kiswahili                               Juma                           anakula ugali.
Kizigua                                  Juma                           adya ugali.
Kisukuma                              Juma                           alelya bugali
Kindali                                   Juma                           akulya            ubbugali.
Kijita                                      Juma                           kalya  ubusima.
Kindendeule                         Juma                           ilye ughale.
 (c)      Ngeli za Majina
Wanataalamu wanakubaliana kuhusu ngeli za majina kwa mujibu wa:
maumbo ya nomino (umoja na wingi wa majina) pamoja; na
upatanisho wa kisarufi katika sentesi.

Kigezo cha maumbo ya majina: Kigezo hiki hufuata maumbo ya umoja na uwingi katika kuyaainisha majina. Majina yaliyo mengi katika lugha ya Kiswahili na lugha za ki-Bantu hufuata mkondo wa umoja na uwingi. Majina ya lugha ya Kiswahili na lugha za ki-Bantu yaliyo mengi yana maumbo dhahiri ya umoja na uwingi.


Mfano:
Lugha za Kibantu               Umoja                        Wingi
Kiswahili                               mtu                 -           watu
                                                mtoto              -           watoto
Kikurya                                  omanto           -           banto (abanto)
                                                omona                        -           bana    (abana)
Kizigua                                  mntu               -           bhantu
                                                mwana            -           bhana
Kindali                                   mundu            -           bhandu
                                                mwana            -           bhana
Kindendeule                         mundu            -           βhandu
                                                mwana            -           βhana

Kigezo cha upatanisho wa kisarufi katika sentesi:
 Katika kigezo hiki tunaangalia uhusiano uliopo kati ya kiima (jina na viambishi awali vya nafsi) na vivumishi katika vitenzi vya Kiswahili na ki-Bantu. Vivumishi, majina pamoja na viambishi hivyo vya vitenzi hubadilika kutokana na maumbo ya umoja na uwingi.

Mfano:
Lugha za Kibantu      Umoja                     -                       Wingi
Kiswahili                      Baba analima         -                       Baba wanalima
Kindali                          Utata akulima        -                       Abbatata bbakulima
Kikurya                         Tata ararema          -                       Batata(Tata)bararema
Kijita                             Tata kalima                        -                       Batata abalima
Kindendeule                Tate ilima               -                       Akatate βhilima

(d)       Vitenzi vya Kiswahili na Kibantu
Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya vitenzi vya Kiswahili na vile vya lugha zingine za ki-Bantu. Vipengele vinavyothibitisha uhusiano huu ni: Viambishi, mnyumbuliko, pamoja na mwanzo au mwisho wa vitenzi, kama ifuatavyo:
Viambishi: vitenzi vya lugha ya Kiswahili na vya lugha zingine za ki-Bantu hujengwa na mzizi (kiini) pamoja na viambishi vyake vya awali na vya tamati.
Mfano:
Kiswahili       -           analima          =          a – na – lim -  a
Kiikuyu          -           arerema          =          a    re –  rem–a
Kindali           -           akulima          =            a  - ku    lim – a
                                                                          1  -  2   -  3  -  4
Sherehe:
1   -     Kiambishi awali kipatanishi cha nafsi.
2   -     Kiambishi awali cha njeo (wakati uliopo).
3   -     Mzizi/Kiini.
4   -     Kiambishi tamati.
Mnyambuliko wa vitenzi: Mnyumbuliko wa vitenzi vya Kiswahili hufanana na ule wa vitenzi vya lugha za ki-Bantu.
Mfano:        
Kiswahili       -           kucheka         -           kuchekesha   -           kuchekelea.
Kindali           -           kuseka            -           kusekasha      -           kusekelela.
Kibena           -           kuheka           -           kuhekesha     -           kuhekelea.
Kinyamwezi  -           kuseka            -           kusekasha      -           kusekelela.
Kikagulu        -           kuseka            -           kusekesha      -           kusekelela

Mwanzo wa vitenzi: Vitenzi  vyote vya Kiswahili na vile vya lugha za ki-Bantu huanza na viambishi ambavyo ni viwakilishi vya nafsi, kama ifuatavyo:
Mfano:
Kiswahili       -           Ni-nakwenda
Kihaya           -           Ni-ngenda
Kiyao             -           N-gwenda
Kindendeule -           Ni-yenda
Mwishilizo wa vitenzi: Vitenzi vya lugha za ki-Bantu na Kiswahili huishia na irabu –a.
Mfano:
Kiswahili       kukimbi-a      -           kuwind-a       -           kushuk-a
Kindali           kukind-a        -           kubhing-a      -           kukol-a
Kisukuma      kupil-a           -           kuhwim-a      -           Kutend-a
Kisunza          kwihuk-a       -           kuhig-a           -           kising-a
Kindendeule kuβhutuk-a    -           kuhwim-a      -           kuhuk-a

Utafiti wa Prof. Maganga kuhusu ushahidi wa ki-Isimu wa kuthibitisha kama Kiswahili ni ki-Bantu au la ungeweza kuelezwa kimuhtasari kwa mifano mingine ifuatayo:

Katika mfano huu inaonekana kwamba mpangilio wa maneno katika sentesi una ufanano kwa sababu katika kila sentesi kuna kiima na kiarifu. Katika kiima kuna nomino, yaani jina la mtenda (Jongo) na katika kiarifu kuna kitendo kinachofanyika na nomino mtendwa. Pia nafasi ya viunganishi ni ile ile kwa lugha zote zilizoonyeshwa katika mfano huu.

Kuna mfano mwingine wa ufanano wa mpangilio huu.

Mfano wa 2:

Lugha
           
Sentesi
Kiswahili
Kihaya
Kisukuma
Kinyaturu
Kipare
Kizigua
           
Sitamkuta kesho
Timushangemu nyenkya
Natusanga intondo
Tumuhanga fadyu
Nesikemkiche yavo
Sirambila luvi

Katika sentensi hizo mpangilio wa maneno una ufanano kwa sababu kila sentensi ina kiima na kiarifu chenye kitenzi na kielezi. Pia kiambishi cha nafsi cha nomino ya mtenda kinajitokeza mwanzoni mwa neno la kwanza la kila sentesi.
Sitamkuta;     Timushangemu;        Natusanga;                                                                            Tumuhanga;            Nesikamkiche;                      Sitambila.

Viambishi hivyo vya nafsi ya mtenda pia vinaonyesha hali ya ukanushi katka kila sentesi na nafasi yake ni ile ile kwa kila sentesi.

Viambishi vya urejeshi navyo vinajitokeza katika kitenzi cha kila sentesi.

Viambishi {m}, {m}, {ti}, {tu} sitamkuta, timushangemu, natusanga, tumuhanga, nesikamkiche, na sitambwila ni vya urejeshi; vinawakilisha nomino mtendwa.

Kwa hivyo, hali hii inadhihirisha kwamba miundo ya sentensi hizi inafanana na vitenzi vyake vina tabia mbalimbali, kama vile:

(i)        kubeba viambishi vya nafsi, mtenda na mtendwa,

(ii)       kuonyeshga hali ya ukanushi njeo za wakati na kitendo kinachofanyika.




Mfano wa 3:
Lugha                     Sentesi
           
Kiswahili        Akija mwambie anifuate
Kizigua
Kihaya
Kisukuma
Kinyaturu
Kipare
Kindendeule
           

Katika sentesi hizo inaonekana kwamba sentesi zote zinafanana  kimpangilio. Pia maneno yake yanakubali uambishaji, kwa mfano:

(i)        Katika maneno ya mwanzo:
            akija, akeza. kalaija, akuja, newaja, ekiza, herufi zilizopigiwa vistari ni viambishi vya nafsi vinawakilisha dhana ya mtenda.

(ii)       Vivyo hivyo katika maneno:
anifuate, ampondele, anitimile, ang’nge, aniratere, angobhekeraye, viambishi vilivyoko katika viarifu vya sentesi hizo vinawakilisha nafsi za watenda.

(iii)     Pia vitenzi vya sentesi hizo vina tabia ya kubeba virejeshi vya nafsi kama ilivyo katika, mwambie, omugambile, nahali,mbwele na umti, vinaonyesha njeo na hali ya uyakinifu- hali inayoonyesha ufanano wa maumbo ya maneno.

(iv)      Licha ya kuwa na mpangilio unaofanana na wa lugha nyingine za kibantu, kwa mfano, katika mifano tuliyoiona hapo juu, baadhi ya maneno yanafanana: tazama maneno:
            kafugha (Kindamba); nafuga  (Kihaya)  nifuga (Kindendeule); anafuga  (Kiswahili).Pia maneno
            nkuku  (Kipare);                   nguku (Kindamba);
            nguku   (Kichaga);               enkoko  (Kihaya);
            ng’uku   (Kikaguru);                        nguku(Kindendeule);
            nguku    (Kindendeule)

Katika mfano wa 3, maneno yafuatayo yana ufanano:

Akeza  (Kizigua);                kalaija   (Kihaya);    alize  (Kisukuma),
newaja  (Kinyaturu);           ekiza   (Kipare);       anda ahikite,... (Kindendeule);
akija,  (Kiswahili.)

Pia maneno;
umugambe   (Kizigua);        omugambile  (Kihaya);       unongeraye (Kindendeule);  na mwambie (Kiswahili).
Ufanano huu wa msamiati, maumbo ya maneno pamoja na wa mpangilio wa maneno katika sentesi, vyote vinathibistisha kwamba lugha ya Kiswahili ni ya kibantu kama zilivyo nyingi nyinginezo.
(ii)    Ushahidi wa Kihistoria Kwamba Kiswahili ni Kibantu
Baada ya kuangalia ushahidi wa kiisimu kuhusu asili ya Kiswahili, katika sehemu hii Maganga (1997) aliendelea kuchambua ushahidi wa Kihistoria unaothibitisha kuwa lugha ya Kiswahili ilizungumzwa katika upwa wa Afrika Mashariki hata kabla ya ujio wa wageni kama vile Waarabu na Wazungu. Ushahidi huu ulitolewa na wageni mbalimbali waliofika hapa Afrika Mashariki. Wote wanathibitisha kuwa lugha ya Kiswahili ilizungumzwa hapa Afrika Mashariki kabla ya ujio wa wageni.
(a)    Ugunduzi wa Ali-Idris (1100-1166)
Ugunduzi huu yasemekana ulifanywa huko Sicily yapata mwaka 1100-1166. Kwenye mahakama ya mfalme Roger II. Licha ya kufahamika kuwa Kiswahili, kilipata kuandikwa kabla ya 10BK. Ali-Idris alikuwa wa kwanza kugundua jina la zamani la Zanzibar kuwa ni Unguja. Katika maelezo yake anaandika pia majina kama vile kikombe, mkono wa tembo, muriani, na kisukari, ambayo ni ya ndizi mbalimbali zilizokuwa zikipatikana huko.


(b)    Ushahidi wa Marco Polo
Huyu ni mzungu ambaye alijishughulisha sana na masuala mbalimbali ya kijiografia na alisafiri sehemu nyingi duniani. Marco Polo aliandika hivi:
“Zanzibari ni kisiwa kizuri ambacho kina ukubwa wa mzunguko wa maili 200. Watu wote wanaabudu (Mungu), wana Mfalme na wanatumia lugha yao, na hawalipi kodi (ushuru) kwa mtu.” Safari za Marco Polo 1958:301
Marco Polo anasemekana aliandika pia kitabu cha jiografia ambacho hakikupata kuchapishwa lakini sehemu zake zimepata kufasiriwa kwa Kirusi na Kifaransa. Mfano mmojawapo ni huu unaofuata:
“Katika visiwa vya Sjawaga vilivyoshughulikiwa katika sura hii, ni kile kisiwa cha Andjaba ambacho mji wake mkuu unaitwa katika lugha ya kwao. Zanguabar/Ungudya, na wakazi wake, japokuwa ni mchanganyiko, kwa sasa wengi wao ni Waislam…chakula chao kikuu kikiwa ndizi. Kuna aina tano ambazo zinajulikana kama kundi, fili, ambazo uzito wake waweza kuwa wakia 12, Omani, Marijani, Sukari....”
Maelezo haya ya Marco Polo yanathibitisha mambo ya msingi kuhusu wakazi wa Pwani ya Afrika ya Mashariki na lugha yao; mintarafu ya dini, chakula na utamaduni wao kwa ujumla.

(c)    Ushahidi wa Al-Masudi (915 BK)
Katika moja ya maandiko yake, Al-Masudi anazungumzia juu ya wakazi wa mwambao ambao walijulikana kwa jina la “wazanji”. Kwa dhana hii, neno Zanzibar linatokana na Zenzibar yaani “Pwani ya Zenji”. Katika maelezo yake Al-Masudi anaonyesha kwamba Wazenji walikuwa  “Watawala Wakilimi” ambao waliaminiwa kuwa walitawala kwa nguvu za Mungu. Kuna maelezo kuwa huenda neno “wakilimi” lina maana ya “wafalme”. Al-Masudi alisisitiza katika maelezo yake kuwa Wazenji walisema lugha kwa ufasaha na walikuwa na viongozi waliowahutubia kwa lugha yao. Kutokana na neno “zenji” kuna uwezekano kuwa kabla ya majilio ya Waarabu, Kiswahili kiliitwa “Kiazania” au “Kizanji” na wageni waliofika pwani.

(d)     Ushahidi wa Ki- Historia wa Mji wa Kilwa
Kimsingi habari zinazoeleza historia ya mji wa Kilwa katika karne ya 10-16BK zinataja majina ya utani kama vile: mkoma watu, nguo nyingi, nk. ambayo walipewa Masultani wa kwanza wa Kilwa Ali Ibn Hussein na mwanae Mohamedi Ibn Ali. Kutokana na habari hizi huenda lugha ya Kiswahili ilishaanza kusemwa mnamo karne ya 10 au ya 11 BK. Maelezo ya kihistoria yanaeleza juu ya Sultani aliyeitwa Talt Ibin Al Husaini ambaye alipewa jina la utani “Hasha Hazifiki”.
 (e)      Utenzi wa Fumo Liyongo (13 BK) kama Ushahidi
Shairi la zamani kabisa lililopata kuandikwa la Kiswahili, linalojulikana ni lile la Utenzi wa Fumo Liyongo. Utenzi huu inasemekana uliandikwa karne ya 13BK. Kuweko kwa shairi hili kunadhihirisha kuwako kwa lugha ya Kiswahili kabla ya karne hiyo, na kwa hivyo, huenda Kiswahili kilianza kutumika kabla ya karne ya 10BK. Baadhi ya beti za utenzi wa Fumo Liyongo ni hizi zifuatazo:
Ubeti  6:         Liyongo Kitamkali,
                        Akabalighi vijali
                        Akawa mtu wa kweli
                        Na hiba huongeya.

Ubeti 7:          Kilimo kama mtukufu
                        Mpana sana mrefu
                        Majimboni yu maarufu
                        Watu huja kwangaliya.

Ubeti 10:        Sultani pate Bwana
                        Papo nae akanena
                        Wagala mumemwona
                        Liyongo kiwatokeya.

3 Bora Zangu

Inayotazamwa Sana

Jinsi Ya Kuufanikisha Mwaka 2017

Mpenzi msomaji wa Makala zangu kwanza kabisa nachukua fursa hii kuwashukuru wote mnaofuatilia Blog yangu,Naomba niwatakie heri ya Mwaka Mpya...

Watazamaji Wangu