Wanawake sita wakazi wa Kata ya Dongobesh wilayani Mbulu wamemtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa kuwachukulia hatua za kisheria askari kadha wa Kituo kidogo cha Polisi Dongobesh akiwemo Mkuu wa Kituo hicho kwa madai ya kuwapiga na kusababisha baadhi yao mimba zao kuharibika.
Wakizungumza mbele ya Mkuu Wilaya hiyo, Anatoli Choya akina mama hao akiwemo Bibi Kizee wa miaka 85 anayefahamika kwa jina la Fabrinia Gusolo, walidai kwamba Polisi hao wakiongozwa na Mkuu huyo wa Kituo cha Mbulu, waliwafuata majumbani kwao na kuwashambulia mapema Wiki iliyopita, kwa madai kuwa akinamama hao walishiriki katika kikao cha mila cha Jamii ya Wairaq kinyume cha taratibu.
Katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Dongobesh, Akina mama hao pia walimueleza Mkuu huyo wa wilaya kuwa kutokana na shambulio hilo lililofanyika kuanzia saa sita za usiku, baadhi yao walitokwa na damu katika sehemu zao za siri kwa muda wa siku tatu huku wakiwa chini ya ulinzi wa Polisi Kituo cha Mbulu.
Huku akitokwa machozi mbele ya Mkuu huyo wa Wilaya, mmoja wanawake hao aliyejitambulisha kwa jina la Scola James ambaye pia anasumbuliwa na kifafa alisema pamoja na kipigo hicho, Polisi hao walimdhalilisha kwa kumvua nguo na kubakiwa na nguo za ndani tu.
Aliongeza kudai kwamba kutokana na kuzuiliwa kituoni hapo kwa siku tatu, mtoto wake wa mwaka mmoja alilazimika kuacha kunyonya kutokana na kuwa mbali na mama yake kwa siku tatu.
Naye Yasinta Amosi akizungumzia hali hiyo alisema Polisi hao wanaume ambao hawakuwa wamefuatana na Polisi yeyote mwanamke waliwadhalilisha wanawake hao kwa kuwashika kwa mtindo wa ‘Tanganyika Jeki’ hali ilyosababisha baadhi yao kubakia uchi.
“Hata kama sisi tulikuwa na makosa walipaswa polisi wa kike waje kutukamata lakini sheria hiyo haikufuatwa na sasa baadhi yetu mimba zao zimetoka na wengine kuharibika kutokana na kukanyagwa na polisi usiku huo”, alilalamika Yasinta.
Akijibu tuhuma hizo, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Anatory Choya, aliwaambia wanawake hao kwamba tuhuma zao zitachunguzwa na kwamba iwapo kutabainika baadhi ya askari hao kuwadhalilisha wanawake hao hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Kuhusu mimba zilizoharibika kutokana na kipigo hicho Mkuu huyo wa Wilaya ya Mbulu aliwataka wale wote ambao mimba zao zimeharibika wafike kituo cha Polisi Mbulu na kufungua mashitaka dhidi ya askari hao iwapo wanawafahamu.
“Naagiza kuwa kama mnawafahamu askari hao kafungueni kesi na kama polisi watawakatalia kufanya hivyo njooni ofisini kwangu tutakwenda na mimi siwezi kuona kazi zinafanywa kinyume halafu ninyamaze” alifoka Mkuu huyo wa wilaya.
Pia Mkuu huyo wa Wilaya ya Mbulu amemuagiza Mkuu wa Polisi wilaya ya Mbulu kumpatia maelezo ni kwa nini hakuwa na askari wa kike katika tukio hilo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa ameahidi kufuatilia tatizo hilo na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika.
CHANZO CHA HABARI KUTOKA GAZETI LA "KUTOKA ARUSHA" TOLEO LA 32
Tanzania Kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Kikanda wa Baraza la Viwanja vya Ndege
Afrika 2025
-
*Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa,akiongea na waandishi wa habari
juu yaMkutano wa Kikanda wa Baraza la Viwanja vya Ndege Afrika *
Na Woinde S...
1 day ago
No comments:
Post a Comment