Ndani ya hifadhi ya Momela-Arusha- Tanzania
Kiswahili Asili Yake ni Kongo
Baadhi ya wataalamu hudai kuwa asili ya lugha ya
Kiswahili ni huko Kongo ambayo baadaye iliitwa Zaire na sasa inaitwa Jamhuri ya
Demokrasia ya Kongo. Dai hili linaimarishwa na wazo lingine linalodai kwamba
katika vipindi kongwe vilivyopata kuwako, sehemu za Pwani ya Afrika mashariki
hazikuwa zimekaliwa na watu. Kutokana na hali ya vita, uchungaji na biashara,
inadaiwa kuwa Wabantu walitoka sehemu za Kongo walisambaa na kuja pwani ya
Afrika mashariki kupitia Kigoma. Baadhi ya wabantu hawa walipitia sehemu za
Uganda. Wakati wa kusambaa kwao, walieneza pia lugha zao ikiwemo hii ya
Kiswahili.
Udhaifu wa nadharia hii ni kwamba, madai ya kuwa
asili ya Kiswahili ni Kongo hayana msingi kwani mpaka sasa wataalamu wanaodai
hivi hawajaweza kueleza na kuthibitisha kisayansi ama Kihistoria juu ya lini
hasa watu walianza kuishi pwani ya Afrika mashariki.
Kiswahili ni Ki-Pijini au ni Ki-Krioli
(i) Kiswahili ni Ki-Pijini
Baadhi ya wataalamu hudai kuwa Kiswahili ni
Ki-Pijini. Wataalamu hawa hudai kwamba Ki-Pijini ni lugha ambayo huzaliwa
kutokana na kukutanika kwa makundi
mawili (A) na (B) yanayotumia lugha mbili tofauti. Ili makundi haya yaweze kuwasiliana
kunaundwa lugha ambayo kitabia ni tofauti
na zile zinazozungumzwa na makundi yanayohusika. Lugha hii inaweza kuwa
na msamiati mwingi kutoka lugha kati ya zile mbili, au inaweza kuwa na msamiati
wenye uzito sawa. Lugha hiyo ndiyo inayoitwa Ki-Pijini. Mazingira
yanayosababisha kuwepo Ki-Pijini ni kama vile biashara, utumwa, ukoloni, nk.
Kwa mantiki ya nadharia hii, wataalamu hawa hukiona
Kiswahili kuwa kilianza kama Ki-Pijini kwani ni tokeo la mwingiliano baina ya
wenyeji wa pwani ya Afrika Mashariki na wageni wa kutoka Mashariki ya Kati,
hususan Waarabu. Aidha, husisitiza kuwa lugha ya Kiswahili haikuwepo kabla ya
hapo.
(ii) Kiswahili ni Ki-Krioli
Wataalamu hawa wanadai kwamba watu wanaozungumza Ki-
Pijini wanaweza kuishi pamoja kwa muda wa karne nyingi na kwa hiyo wakaweza
kuzoeana na hata kufikia hatua ya kuoana. Wakioana watoto wao huikuta lugha ya
ki-Pijini ama lugha yao ya kwanza. Inapofikia hatua ya aina hii kwa watoto
wanaozungumza lugha hiyo, wao husemekana sasa
wanazungumza lugha ya Ki-Krioli, lugha ambayo ni hatua ya juu ya
Ki-Pijini, yaani Ki-Pijini kilichokomaa.
Nadharia hii hutumia kigezo cha msamiati wa
Kiswahili kuonesha uhusiano uliopo kati ya Kiswahili na Kiarabu. Wanadai kuwa,
msamiati mwingi wa Kiswahili unatokana na Kiarabu. Hivyo huhitimisha kuwa
hapana shaka Kiarabu kimehusika katika kuizalisha na kuikomaza lugha ya
Kiswahili.
Udhaifu wa nadharia hii ni kwamba hutumia kigezo cha
msamiati tu bila kuzingatia vipengele vingine vya lugha kama vile matamshi,
maumbo ya maneno au muundo wa sentensi za Kiswahili. Aidha, wataalamu hawa
hawakuhoji suala la kufanana kwa Kiswahili na lugha jirani katika hayo
yaliyotajwa hapo juu na katika eneo la Kijografia ambamo Kiswahili na lugha
hizo nyingine hujikuta zikizungumzwa. Vigezo hivi ni ushahidi tosha unaoonesha
kuwa Kiswahili SI Ki-Pijini wala SI Ki-Krioli, bali ni lugha kama zilivyo hizo
lugha jirani.
Kiswahili ni Lugha ya Jamii ya Vizalia
Kundi la kwanza la wataalamu wa nadharia hii, Bishop
Edward Steera, Bwana Taylor, Dkt. R. Reusch, (Katika Maganga, 1997) hudai kwamba:
·
Waarabu na Waajemi waliohamia pwani ya Afrika ya Mashariki waliwaoa
wanawake wa ki-Afrika.
·
Watoto wao walijifunza maneno ya Kiarabu na ki-Ajemi kutoka kwa baba
zao.
·
Aidha, watoto hao wakajifunza maneno ya ki-Bantu kutoka kwa mama zao.
·
Katika jitihada zao, watoto hao walijirekebisha kutokana na tamaduni za wazazi wao ambazo ni tafauti:
utamaduni wa Kiarabu na utamaduni wa ki-Bantu.
·
Vizalia hawa wakaanza kutumia lugha mpya ya mseto wa Kiarabu, Kiajemi na
lahaja mbalimbali za ki-Bantu.
· Kwa
kiasi kikubwa, lugha mpya ya mseto ilikuwa ni upotoshaji wa lugha ya Kiarabu na
Kiajemi.
·
Mwarabu au Mu-Ajemi alikuwa muumini wa dini ya Uislamu.
· Umo
humo, vizalia hawa wakayaingiza maneno ya Kiarabu, Kishirazi na Kihindi katika
hii lugha mpya.
·
Pamoja na kuyaingiza maneno ya kigeni, lugha-mpya yao hii (Kiswahili),
ilikithiri vionjo vingi vya lugha mbali mbali za ki-Bantu.
· Ndipo
baadaye, lugha mpya yao hii ikajulikana au kuitwa Kiswahili.
· Kwa
maoni ya wataalamu hawa, sehemu mbili kati ya tano (2/5) ya maneno yanayotumika
katika lugha hii mpya ni ya ki-Bantu.
·
Sarufi ya lugha mpya hii ni mseto wa ki-Bantu (chenye utata na kisicho
na mpangilio maalumu) pamoja na Kiarabu (chenye mantiki na kilichokomaa).
Kundi la pili la wataalamu wa nadharia hii, B. Krumm
na F. Johnson lina mawazo yanayodai kwamba:
·
Kiswahili kilitokana na visiwa vya Lamu, Kilamu/Kiamu.
·
Wageni kutoka Ghuba ya Ushirazi/Uajemi na Arabia ya Kusini walikuja
katika Pwani ya Afrika ya Mashariki na lugha tofauti.
·
Lakini kutokana na kuoana kwao na wenyeji, wageni hawa wakaichukua lugha
ya hapo walipofikia, wakaikuza kwa maneno kadhaa na sentensi kadhaa kutoka
lugha zao za asili, yaani Kiarabu, Kiajemi na Kihindi hususan katika masuala
ya biashara, ubaharia, vyombo vya kazi
zao na nguo.
·
Aidha, utumwa na tabia ya kuoa
wake wengi ilisaidia kutoa kundi kubwa la masuria. Hali hii ikaondosha hisia za
ugeni katika lugha zao; na maneno yote yakabatizwa kuwa ya ki-Bantu, na hata
kupoteza kabisa sura ya ugeni.
Kiswahili ni Kiarabu
Kuna hoja kuu tatu ambazo baadhi ya wananadharia hii
huzitumia kutetea nadharia hii kuwa Kiswahili asili yake ni Kiarabu.
(i)
Inadaiwa kuwa maneno yenye asili ya Kiarabu yaliyomo katika Kiswahili ni
ishara tosha kwamba lugha hii ilianza kama Pijini ya Kiarabu.
(ii)
Inahusu neno lenyewe Kiswahili ambalo asili yake ni Kiarabu. Neno
Kiswahili linatokana na neno “sahili” (umoja) na “swahil” (wingi) lina maana ya
pwani.
(iii)
Inadaiwa kwamba kwa kuwa Kiswahili kilianza pwani, kwa kuwa idadi kubwa
sana ya wenyeji wa pwani ni waislamu, na kwa kuwa uisilamu uliletwa na Waarabu,
basi Kiswahili nacho kililetwa na Waarabu.
Kiswahili si Kiarabu
Madai kwamba Kiswahili si Kiarabu yanathibitishwa na
hoja kinzani zifuatazo:
Tukianza na dai la kwanza ‘kwamba maneno yenye asili
ya Kiarabu yaliyomo katika Kiswahili ni ishara tosha kwamba lugha hii ilianza
kama pijini ya Kiarabu’ tunaona wazi kwamba madai haya hayana mashiko. Lugha ya
Kiswahili imetokea kuwa na maneno ya mkopo yenye asili ya Kiarabu (na kwa
hakika yapo yenye asili ya Kiajemi, Kireno, Kihindi, Kijerumani, Kiingereza
kutokana na
ukweli kwamba kulikuwa na mawasiliano ya karne na karne baina ya wenyeji wa
pwani na wafanyabiashara wa Kiarabu. Wasemaji wa lugha mbili tofauti
wanapokutana hawaachi kuathiriana kilugha. Kwa hiyo lugha kuwa na maneno mengi
ya mkopo kutoka lugha nyingine, haifanyi lugha hiyo isemekane kuwa imetokana na
hiyo lugha nyingine.
Pili wataalamu hawa wanadai kwamba neno lenyewe
Kiswahili lina maana ya Kiarabu.
Kwani linatokana na neno “sahili” (umoja) na
“swahil” (wingi) lina maana ya pwani. Hapa ingetupasa tuelewe kwamba kila mtu binafsi
au jamii binafsi aghalabu hajiiti mwenyewe jina lake, yeye huitwa kwa hilo jina
alilopewa na wengine: Jamii yake au wageni waliomtembelea kwake. Na hivi ndivyo
ilivyojitokeza kwa upande wa jamii ya watu wa pwani ya Afrika mashariki, yaani
Waswahili, walipotembelewa na Waarabu na
kuitwa As-Sahilyy au As-Sawahiliyy, na nchi yao kuitwa sahil (wingi wake
Sawahil), yaani pwani (upwa), ufuo. Kwa mantiki hii, dai hili halina mashiko !
Kigezo cha dini nacho hakikubaliki lugha haiwi lugha
kwa sababu ya imani. Hata hivyo lugha ya Kiarabu yenyewe ilikuwepo karne nyingi
kabla ya kufunuliwa dini ya Uislamu. Hali kadhalika, lugha nyingine za
Kimagharibi zilikuwepo karne nyingi kabla ya kufunuliwa imani ya ukristo. Kama
ilivyo kwamba Kiingereza au Kijerumani si ukristo, basi ndivyo vivi hivyo
ilivyo kwamba Kiswahili hakiwezi kuwa dini ya uislamu, aslan! Wala Kiarabu
nacho si uislamu. Tunachoweza kufanya ni kuitumia lugha kuifasili dini, lakini
hatuwezi kuitumia dini kuifasili lugha.
Kiswahili ni Kibantu
Vipengele vinavyotumika katika kuihalalisha nadharia
inayodai kwamba Kiswahili ni Kibantu ni ushahidi wa ki-Isimu, ushahidi wa
ki-Historia na kuichunguza lugha ya Kiswahili katika mfumo mzima wa historia ya
mgawanyiko wa kusambaa kwa lugha za ki-Bantu. Wataalamu wa nadharia hii
wanahitimisha kwa kudai kwamba Kiswahili ni mojawapo kati ya lugha katika jamii kubwa ya lugha za
ki-Bantu.
Baadhi ya wataalamu muhimu wanaoiunga mkono nadharia
hii ni Prof. Malcon Guthrie, Dkt. C. Meinholf na Dkt. C. Rohl na Prof. Clement
Maganga.
Profesa
Malcom Guthrie
Ni mtaalamu
(mwanaisimu) mashuhuri kutoka Chuo Kikuu cha London, Uingereza. Alitumia miaka
20 kuchunguza uhusiano uliopo baina ya lugha za Kibantu zilizoko katika eneo
lote ambalo hukaliwa na wabantu. Sehemu hii ni ile ambayo inajulikana kama
Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Alifanya uchunguzi wa mashina/mizizi (viini) ya
maneno 22,000 kutoka lugha 200 za Kibantu. Katika uchunguzi wake alikuta mizizi
(mashina) 2,300 imezagaa katika
lugha mbalimbali za Kibantu na Kiswahili kikiwemo. Mashina/mizizi 500yalilingana
katika lugha zote 200. Mashina haya yalipatikana katika lugha zote za Kibantu.
Mashina haya yalikuwa ya asili moja. Baadhi ya lugha hizo 200 zilizofanyiwa
uchunguzi Kiswahili kilionesha kuitikia ulinganifu sawa na Kikongo kwa asilimia
arubaini na nne (44%).
Katika kuchunguza ni asilimia ngapi za mashina hayo
500 yaliyomo katika kila lugha, mgawo uliojitokeza ulikuwa kama ifuatavyo:
Kiwemba kizungumzwacho Zambia - 54%
Kiluba kizungumzwacho Katanga - 51%
**Kikongo kizungumzwacho Zaire - 44%**
**Kiswahili kizungumzwacho Afrika Mashariki 44%**
Kisukuma kizungumzwacho Tanzania 41%
Kiyao kizungumzwacho Tanzania/Msumbiji - 35%
Sotho kizungumzwacho Botswana - 20%
*Kirundi kizungumzwacho Burundi - 43%*
Kinyoro kizungumzwacho Uganda - 37%
Kizulu kizungumzwacho Afrika Kusini -
29%
Baada ya kupata matokeo haya, Profesa Malcom Guthrie
anaiunga mkono nadharia hii ya kwamba Kiswahili ni ki-Bantu kwa kudai kwamba:
(i)
Kiswahili kilikuwepo kabla ya ujio wa wageni;
(ii)
Anaonyesha kwamba Kiswahili kina uhusiano mkubwa na lugha za Kibantu;
(iii) Mwisho
anasema Kiswahili kilianzia Pwani ya Afrika Mashariki.
Dkt.
C. Meinholf na Dkt. C. Rohl: Wataalamu hawa wanaamini kwamba:
(i) Wakati wa
utawala wa Shirazi katika upwa wa mashariki ya Afrika kulikuwa na kabila la
Waswahili;
(ii) Kabila hili ni dhuria ya Wazaramo wa
leo.
(iii)
Kwa kuwa hawa Wazaramo walikuwa wamezaliwa katika harakati za
kibiashara, kwa hivyo wakafuata nyayo za wazazi wao.
(iv)
Lugha yao ilikuwa ya aina ya ki-Bantu.
(v)
Kwa kuwa Wabantu ni wengi zaidi kuliko jamii ya makabila mengine, lugha
yao ya Kiswahili ikaanza kutumika na kuenea katika makabila mengine, hususan
katika ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki.
(vi)
Baadaye, Waswahili hawa hawa wakafanya biashara na wageni waliokuja
kuvinjari Afrika Mashariki, hususan Waarabu, Washirazi, Wamalaysia, Wahindi na
Wareno ambao tayari walikuwa wamefurika katika pwani hii ya Afrika Mashariki
miaka kadhaa kabla.
(vii)
Vifaa na majina ya vitu vya biashara vya wageni hao vikaselelea na
kuingizwa katika mfumo wa lugha hiyo ya Waswahili ambayo ni ki-Bantu.
Madai ya nadharia hii yakichunguzwa, tunagundua
kwamba inazingatia mitazamo miwili yaani, mtazamo wa ki-Isimu na mtazamo wa
ki-Historia. Kwa mantiki hii, nadharia hii inaelekea kukubalika na wataalamu
wengi kuwa ndiyo sahihi kuhusu asili au historia ya Kiswahili.
Profesa C. Maganga, na uthibitisho wake kwamba
Kiswahili ni ki-Bantu. Kama tulivyoona, lugha ya Kiswahili ilifanyiwa utafiti
na uchambuzi na wanataaluma kadhaa kwa madhumuni ya kuiainisha kama ilikuwa
yenye misingi ya ki-Bantu au la. Prof. Maganga alifanya uchambuzi wa ki-Isimu
na wa ki-Historia kuhusu lugha hii. Matokeo ya utafiti wake wa ki-Isimu kuhusu
lugha ya Kiswhili (au lugha kwa ujumla) unadhihirisha mambo mengi, mojawapo ni
asili ya lugha hiyo. Amethibitisha kwamba Kiswahili ni lugha ya Kibantu; na kwa
hivyo, kuthibitisha kwa ushahidi thabiti hoja ya Dkt. C. Meinholf na Dkt. C.
Rohl kama tulivyoieleza hapo juu.
(i) Ushahidi wa Kiisimu
(a)
Msamiati
Matokeo ya utafiti alioufanya kuhusu msamiati wa
Kiswahili ulibaini kwamba 60% ya maneno yote yanayoweza kuandikwa na kutamkika
katika lugha ya Kiswahili asili yake ni lugha za Kibantu, 30% ni lugha ya
Kiarabu na 10% ni lugha nyingine za kigeni kama vile Kiingereza, Kireno,
Kijerumani, Kihindi, Kiajemi, Kifaransa, nk. Kinyume chake ni kwamba msamiati
wa Kiswahili na ule wa Kibantu hautofautiani.
Mfano:
Kiswahili Kindali
Kizigua Kijita Kikurya
Kindendeule
Mtu Umundu Mntu
Omun Omontu Mundu
Maji Amashi Manzi
Amanji Amanche Maache
Moto Umulilo Moto
Omulilo Omoro Mwoto
(b)
Tungo (Sentesi) za Kiswahili
Miundo ya tungo (sentesi) za maneno ya Kiswahili
zinafanana sana na miundo ya tungo za maneno ya ki-Bantu. Sentesi za Kiswahili
na za lugha za ki-Bantu zina kiima na
kiarifu.
Mfano:
Lugha
za Kibantu Kiima kiarifu
Kiswahili Juma anakula ugali.
Kizigua Juma adya ugali.
Kisukuma Juma alelya bugali
Kindali Juma akulya ubbugali.
Kijita Juma kalya ubusima.
Kindendeule Juma ilye ughale.
(c)
Ngeli za Majina
Wanataalamu wanakubaliana kuhusu ngeli za majina kwa
mujibu wa:
maumbo ya nomino (umoja na wingi wa majina) pamoja;
na
upatanisho wa kisarufi katika sentesi.
Kigezo cha maumbo ya majina: Kigezo hiki hufuata
maumbo ya umoja na uwingi katika kuyaainisha majina. Majina yaliyo mengi katika
lugha ya Kiswahili na lugha za ki-Bantu hufuata mkondo wa umoja na uwingi.
Majina ya lugha ya Kiswahili na lugha za ki-Bantu yaliyo mengi yana maumbo
dhahiri ya umoja na uwingi.
Mfano:
Lugha
za Kibantu Umoja Wingi
Kiswahili mtu - watu
mtoto - watoto
Kikurya omanto - banto (abanto)
omona
- bana (abana)
Kizigua mntu - bhantu
mwana - bhana
Kindali mundu - bhandu
mwana - bhana
Kindendeule mundu - βhandu
mwana - βhana
Kigezo
cha upatanisho wa kisarufi katika sentesi:
Katika kigezo
hiki tunaangalia uhusiano uliopo kati ya kiima (jina na viambishi awali vya
nafsi) na vivumishi katika vitenzi vya Kiswahili na ki-Bantu. Vivumishi, majina
pamoja na viambishi hivyo vya vitenzi hubadilika kutokana na maumbo ya umoja na
uwingi.
Mfano:
Lugha
za Kibantu Umoja - Wingi
Kiswahili Baba analima - Baba wanalima
Kindali Utata akulima - Abbatata bbakulima
Kikurya Tata ararema - Batata(Tata)bararema
Kijita Tata kalima - Batata abalima
Kindendeule Tate ilima - Akatate βhilima
(d) Vitenzi vya Kiswahili na Kibantu
Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya vitenzi vya
Kiswahili na vile vya lugha zingine za ki-Bantu. Vipengele vinavyothibitisha
uhusiano huu ni: Viambishi, mnyumbuliko, pamoja na mwanzo au mwisho wa vitenzi,
kama ifuatavyo:
Viambishi:
vitenzi vya lugha ya Kiswahili na vya lugha zingine za ki-Bantu hujengwa na
mzizi (kiini) pamoja na viambishi vyake vya awali na vya tamati.
Mfano:
Kiswahili
- analima = a – na – lim - a
Kiikuyu
- arerema = a
– re – rem–a
Kindali
- akulima = a
- ku – lim – a
1 -
2 - 3
- 4
Sherehe:
1 - Kiambishi awali kipatanishi cha nafsi.
2 - Kiambishi awali cha njeo (wakati uliopo).
3 - Mzizi/Kiini.
4 - Kiambishi tamati.
Mnyambuliko
wa vitenzi: Mnyumbuliko wa vitenzi vya Kiswahili hufanana
na ule wa vitenzi vya lugha za ki-Bantu.
Mfano:
Kiswahili
- kucheka - kuchekesha -
kuchekelea.
Kindali
- kuseka - kusekasha - kusekelela.
Kibena
- kuheka - kuhekesha -
kuhekelea.
Kinyamwezi
- kuseka - kusekasha - kusekelela.
Kikagulu
- kuseka - kusekesha -
kusekelela
Mwanzo
wa vitenzi: Vitenzi
vyote vya Kiswahili na vile vya lugha za ki-Bantu huanza na viambishi
ambavyo ni viwakilishi vya nafsi, kama ifuatavyo:
Mfano:
Kiswahili
- Ni-nakwenda
Kihaya
- Ni-ngenda
Kiyao
- N-gwenda
Kindendeule - Ni-yenda
Mwishilizo
wa vitenzi: Vitenzi vya lugha za ki-Bantu na
Kiswahili huishia na irabu –a.
Mfano:
Kiswahili
kukimbi-a - kuwind-a - kushuk-a
Kindali
kukind-a - kubhing-a - kukol-a
Kisukuma
kupil-a - kuhwim-a - Kutend-a
Kisunza
kwihuk-a - kuhig-a - kising-a
Kindendeule kuβhutuk-a -
kuhwim-a - kuhuk-a
Utafiti wa Prof. Maganga kuhusu ushahidi wa ki-Isimu
wa kuthibitisha kama Kiswahili ni ki-Bantu au la ungeweza kuelezwa kimuhtasari
kwa mifano mingine ifuatayo:
Katika mfano huu inaonekana kwamba mpangilio wa
maneno katika sentesi una ufanano kwa sababu katika kila sentesi kuna kiima na
kiarifu. Katika kiima kuna nomino, yaani jina la mtenda (Jongo) na katika
kiarifu kuna kitendo kinachofanyika na nomino mtendwa. Pia nafasi ya
viunganishi ni ile ile kwa lugha zote zilizoonyeshwa katika mfano huu.
Kuna mfano mwingine wa ufanano wa mpangilio huu.
Mfano wa 2:
Lugha
Sentesi
Kiswahili
Kihaya
Kisukuma
Kinyaturu
Kipare
Kizigua
Sitamkuta kesho
Timushangemu nyenkya
Natusanga intondo
Tumuhanga fadyu
Nesikemkiche yavo
Sirambila luvi
Katika sentensi hizo mpangilio wa maneno una ufanano
kwa sababu kila sentensi ina kiima na kiarifu chenye kitenzi na kielezi. Pia
kiambishi cha nafsi cha nomino ya mtenda kinajitokeza mwanzoni mwa neno la
kwanza la kila sentesi.
Sitamkuta;
Timushangemu;
Natusanga;
Tumuhanga;
Nesikamkiche;
Sitambila.
Viambishi hivyo vya nafsi ya mtenda pia vinaonyesha
hali ya ukanushi katka kila sentesi na nafasi yake ni ile ile kwa kila sentesi.
Viambishi vya urejeshi navyo vinajitokeza katika
kitenzi cha kila sentesi.
Viambishi {m}, {m}, {ti}, {tu} sitamkuta,
timushangemu, natusanga, tumuhanga, nesikamkiche, na sitambwila ni vya
urejeshi; vinawakilisha nomino mtendwa.
Kwa hivyo, hali hii inadhihirisha kwamba miundo ya
sentensi hizi inafanana na vitenzi vyake vina tabia mbalimbali, kama vile:
(i)
kubeba viambishi vya nafsi, mtenda na mtendwa,
(ii)
kuonyeshga hali ya ukanushi njeo za wakati na kitendo kinachofanyika.
Mfano wa 3:
Lugha Sentesi
Kiswahili Akija mwambie anifuate
Kizigua
Kihaya
Kisukuma
Kinyaturu
Kipare
Kindendeule
Katika sentesi hizo inaonekana kwamba sentesi zote
zinafanana kimpangilio. Pia maneno yake
yanakubali uambishaji, kwa mfano:
(i)
Katika maneno ya mwanzo:
akija, akeza. kalaija, akuja, newaja, ekiza, herufi zilizopigiwa vistari
ni viambishi vya nafsi vinawakilisha dhana ya mtenda.
(ii)
Vivyo hivyo katika maneno:
anifuate, ampondele, anitimile, ang’nge, aniratere,
angobhekeraye, viambishi vilivyoko katika viarifu vya sentesi hizo
vinawakilisha nafsi za watenda.
(iii) Pia
vitenzi vya sentesi hizo vina tabia ya kubeba virejeshi vya nafsi kama ilivyo
katika, mwambie, omugambile, nahali,mbwele na umti, vinaonyesha njeo na hali ya
uyakinifu- hali inayoonyesha ufanano wa maumbo ya maneno.
(iv)
Licha ya kuwa na mpangilio unaofanana na wa lugha nyingine za kibantu,
kwa mfano, katika mifano tuliyoiona hapo juu, baadhi ya maneno yanafanana:
tazama maneno:
kafugha (Kindamba); nafuga
(Kihaya) nifuga (Kindendeule);
anafuga (Kiswahili).Pia maneno
nkuku (Kipare); nguku (Kindamba);
nguku (Kichaga); enkoko (Kihaya);
ng’uku (Kikaguru); nguku(Kindendeule);
nguku (Kindendeule)
Katika mfano wa 3, maneno yafuatayo yana ufanano:
Akeza
(Kizigua);
kalaija (Kihaya); alize
(Kisukuma),
newaja
(Kinyaturu); ekiza (Kipare); anda ahikite,... (Kindendeule);
akija,
(Kiswahili.)
Pia maneno;
umugambe
(Kizigua); omugambile (Kihaya); unongeraye (Kindendeule); na mwambie (Kiswahili).
Ufanano huu wa msamiati, maumbo ya maneno pamoja na
wa mpangilio wa maneno katika sentesi, vyote vinathibistisha kwamba lugha ya
Kiswahili ni ya kibantu kama zilivyo nyingi nyinginezo.
(ii) Ushahidi wa Kihistoria Kwamba Kiswahili ni
Kibantu
Baada ya kuangalia ushahidi wa kiisimu kuhusu asili
ya Kiswahili, katika sehemu hii Maganga (1997) aliendelea kuchambua ushahidi wa
Kihistoria unaothibitisha kuwa lugha ya Kiswahili ilizungumzwa katika upwa wa
Afrika Mashariki hata kabla ya ujio wa wageni kama vile Waarabu na Wazungu.
Ushahidi huu ulitolewa na wageni mbalimbali waliofika hapa Afrika Mashariki.
Wote wanathibitisha kuwa lugha ya Kiswahili ilizungumzwa hapa Afrika Mashariki
kabla ya ujio wa wageni.
(a) Ugunduzi wa Ali-Idris (1100-1166)
Ugunduzi huu yasemekana ulifanywa huko Sicily yapata
mwaka 1100-1166. Kwenye mahakama ya mfalme Roger II. Licha ya kufahamika kuwa
Kiswahili, kilipata kuandikwa kabla ya 10BK. Ali-Idris alikuwa wa kwanza
kugundua jina la zamani la Zanzibar kuwa ni Unguja. Katika maelezo yake
anaandika pia majina kama vile kikombe, mkono wa tembo, muriani, na kisukari,
ambayo ni ya ndizi mbalimbali zilizokuwa zikipatikana huko.
(b) Ushahidi wa Marco Polo
Huyu ni mzungu ambaye alijishughulisha sana na
masuala mbalimbali ya kijiografia na alisafiri sehemu nyingi duniani. Marco
Polo aliandika hivi:
“Zanzibari ni kisiwa kizuri ambacho kina ukubwa wa
mzunguko wa maili 200. Watu wote wanaabudu (Mungu), wana Mfalme na wanatumia
lugha yao, na hawalipi kodi (ushuru) kwa mtu.” Safari za Marco Polo 1958:301
Marco Polo anasemekana aliandika pia kitabu cha
jiografia ambacho hakikupata kuchapishwa lakini sehemu zake zimepata kufasiriwa
kwa Kirusi na Kifaransa. Mfano mmojawapo ni huu unaofuata:
“Katika visiwa vya Sjawaga vilivyoshughulikiwa
katika sura hii, ni kile kisiwa cha Andjaba ambacho mji wake mkuu unaitwa
katika lugha ya kwao. Zanguabar/Ungudya, na wakazi wake, japokuwa ni
mchanganyiko, kwa sasa wengi wao ni Waislam…chakula chao kikuu kikiwa ndizi.
Kuna aina tano ambazo zinajulikana kama kundi, fili, ambazo uzito wake waweza
kuwa wakia 12, Omani, Marijani, Sukari....”
Maelezo haya ya Marco Polo yanathibitisha mambo ya
msingi kuhusu wakazi wa Pwani ya Afrika ya Mashariki na lugha yao; mintarafu ya
dini, chakula na utamaduni wao kwa ujumla.
(c) Ushahidi wa Al-Masudi (915 BK)
Katika moja ya maandiko yake, Al-Masudi anazungumzia
juu ya wakazi wa mwambao ambao walijulikana kwa jina la “wazanji”. Kwa dhana
hii, neno Zanzibar linatokana na Zenzibar yaani “Pwani ya Zenji”. Katika
maelezo yake Al-Masudi anaonyesha kwamba Wazenji walikuwa “Watawala Wakilimi” ambao waliaminiwa kuwa
walitawala kwa nguvu za Mungu. Kuna maelezo kuwa huenda neno “wakilimi” lina
maana ya “wafalme”. Al-Masudi alisisitiza katika maelezo yake kuwa Wazenji
walisema lugha kwa ufasaha na walikuwa na viongozi waliowahutubia kwa lugha
yao. Kutokana na neno “zenji” kuna uwezekano kuwa kabla ya majilio ya Waarabu,
Kiswahili kiliitwa “Kiazania” au “Kizanji” na wageni waliofika pwani.
(d) Ushahidi wa Ki- Historia wa Mji wa Kilwa
Kimsingi habari zinazoeleza historia ya mji wa Kilwa
katika karne ya 10-16BK zinataja majina ya utani kama vile: mkoma watu, nguo
nyingi, nk. ambayo walipewa Masultani wa kwanza wa Kilwa Ali Ibn Hussein na
mwanae Mohamedi Ibn Ali. Kutokana na habari hizi huenda lugha ya Kiswahili
ilishaanza kusemwa mnamo karne ya 10 au ya 11 BK. Maelezo ya kihistoria
yanaeleza juu ya Sultani aliyeitwa Talt Ibin Al Husaini ambaye alipewa jina la
utani “Hasha Hazifiki”.
(e)
Utenzi wa Fumo Liyongo (13 BK) kama Ushahidi
Shairi la zamani kabisa lililopata kuandikwa la
Kiswahili, linalojulikana ni lile la Utenzi wa Fumo Liyongo. Utenzi huu
inasemekana uliandikwa karne ya 13BK. Kuweko kwa shairi hili kunadhihirisha
kuwako kwa lugha ya Kiswahili kabla ya karne hiyo, na kwa hivyo, huenda
Kiswahili kilianza kutumika kabla ya karne ya 10BK. Baadhi ya beti za utenzi wa
Fumo Liyongo ni hizi zifuatazo:
Ubeti 6: Liyongo Kitamkali,
Akabalighi vijali
Akawa mtu wa kweli
Na hiba huongeya.
Ubeti 7:
Kilimo kama mtukufu
Mpana sana mrefu
Majimboni yu maarufu
Watu huja kwangaliya.
Ubeti 10:
Sultani pate Bwana
Papo nae akanena
Wagala mumemwona
Liyongo kiwatokeya.
No comments:
Post a Comment